DALILI ZA MTU ALIYEFUNGWA NA NGUVU ZA GIZA




DALILI 22 ZA MTU ALIYEFUNGWA NA NGUVU ZA GIZA
1. Kuangalia ovyo ovyo. Hawezi kutuliza macho sehemu moja wala kumuangalia mtu usoni.
2. Kupindua macho kwa namna fulani hivi kana kwamba anataka kuwa na makengeza. Sehemu ya mboni ya jicho ambayo ni nyeusi kwa kiasi fulani hujificha na badala yake sehemu nyeupe inaonekena karibia jicho zima. Macho yanakuwa tofauti kabisa na alivyozoeleka kwa wanao mfahamu.
3. Kuwa na nguvu kupita kiasi. Makao yake yalikuwa pale makaburini; wala hakuna mtu yeyote aliyeweza kumfunga tena, hata kwa minyororo; kwa sababu alikuwa amefungwa mara nyingi kwa pingu na minyororo, akaikata ile minyororo na kuzivunja vunja zile pingu; wala hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda. Marko 5:3-4
4. Maumivu ya tumbo chini ya kitovu yakiambatana na kitu kinachotembea tembea (hasa kwa wanawake). Utamsikia akilalamika sana juu ya maumivu makali chini ya kitovu, ambayo hupotea mara moja pale tu atakapoombewa. Tahadhari iwepo maana hata vidonda vya tumbo na minyoo pia huwa na dalili zinazokaribia kufanana na hii. Hivyo siyo hekima kuamua mara moja kwa dalili hii moja. Kwa kuwa tunaye roho aishiye ndani yetu tumuombe atusaidie kuwa na utambuzi wa kutosha.
5. Kusikia kubanwa (kukabwa kifua au shingo). Mtu ataanza kushindwa kupumua kama ilivyo kawaida. Atalalamika kubanwa au kukabwa huku akipumua kwa shida sana. Hatua zisipochukuliwa mapema hii husababisha mtu kuzimia na hata kukata roho hasa kwa wale wasiojua habari za Mungu aliyehai na namna ya kuitumia damu ya Yesu katika kukemea na kufukuza nguvu hizi za giza. Tahadhari; utambuzi wa roho mtakatifu utumike ili kutofautisha kubanwa kwa aina hii na kule kwa athma.
6. Kuanguka ghafla na kupoteza fahamu. Tahadhari; kuanguka na kupoteza fahamu huweza kusababishwa na magonjwa mengine ya kawaida kama shinikizo la damu, kuzidiwa na malaria au hata kuzidiwa na madawa kama mtu atakuwa ametumia zaidi au akashindwa kula vizuri wakati akiwa kwenye dozi kali au hata kuzidiwa na njaa. Jambo kubwa la kufanya ni kumuombea ili idhihirike wazi. Kama itakuwa ni nguvu za giza dalili itaonekana na kama ni ugonjwa wa kawaida hatua za kumpeleka hospitali zichukuliwe mapema iwezekanavyo baada tu ya kumaliza ombi.
7. Kusikia kuwaka moto kichwani. Si kawaida kwa binadamu asiye na matatizo kusikia kana kwamba kichwa kinawaka moto hasa sehemu za utosini. Nguvu za giza kama zimekimbilia sehemu ya kichwa huweza kusababisha hili na kumyima raha kabisa mgonjwa. Aweza kwenda hospitali sana lakini hakuna ufumbuzi utakaopatika juu ya tatizo hili. Hali itazidi tu kuwa mbaya siku hadi siku.
8. Kusikia kichwa kuwa kizito (kichwa kinakuwa ovyo). Mtu aliyeingiliwa na nguvu za giza aweza kujisikia vibaya kichwani, hata akiulizwa hawezi kutoa maelezo zaidi ya kulalamika tu kuwa anasikia kichwa kiko ovyo au ni kizito na haelewi ni kitu gani. Tahadhari; hii yaweza kusababishwa pia na shinikizo la damu, hivyo tahadhari ichukuliwe kwa utambuzi wa kiroho zaidi.
9. Kuota anafanya ngono na mtu fulani (anaweza akawa anamjua au la). Tahadhari isipochukuliwa mapema nguvu za giza kwa namna hii hufanikiwa kabisa kuvunja ndoa.
10. Kuota unafukuzwa na wanyama wakali. Hii ni dalili ya kuchezewa na wachawi au mizimu
11. Kuoteshwa dawa (mti fulani ni dawa). Hii ni mizimu inayotaka kukutumia kwa habari za uaguzi. Kama mtu atakubaliana na hali hii atakuwa mtumishi wa nguvu za giza na mwenye nguvu sana katika ulimwengu wa giza.
12. Kulia au kucheka ovyo.
13. Kusisimka mwili na kusimama nywele. Ndipo pepo ilipita mbele ya uso wangu; na nywele za mwili wangu zilisimama. Ayubu 4:15. Yapo maeneo ambayo mtu akipita (inaweza kuwa chini ya mti au pembeni mwa jabali n.k) anasimamwa na nywele au hata ndani ya chumba unaweza kusikia upepo wa baridi ukikupitia na nywele zinasimama. Hii huashiria uwepo wa nguvu za giza.
14. Kuhisi vitu vinatembea mwilini. Yaweza kuwa ndani au nje ya mwili; mtu atalalamika kuwa kuna vitu vinamtembelea lakini havioni kwa macho hata mlio karibu hamwezi pia kuviona.
15. Kusononeka na kukosa amani mara kwa mara. Maandiko katika Wafilipi 4:4 yanataja furaha wanayokuwa nayo wale wampendao Bwana na ambao Bwana anaishi ndani yao. Kinyume na hapo kama hakuna sababu ya kibinadamu iliyosababisha mtu kukosa amani basi ujue wazi ni nguvu za giza zilizoleta masononeko hayo. Furahini katika Bwana siku zote; tena nasema, furahini. Wafilipi 4:4.
16. Kusikia uzito wa kichwa, au kichwa kutokuwa katika hali ya kawaida hasa baada ya ndoto. Ndoto inaweza kuwa imesaahulika au inakumbwa, lakini baada ya kushituka usingizini kuna kuwa na hali isiyo ya kawaida kichwani.
17. Kuogopa vitu vidogovidogo.
18. Kuota watu waliokufa mara kwa mara au kutokewa na watu waliokufa. Hii ni nguvu za giza na hasa upande wa mizimu.
19. Kuwepo chuki kwa wanandoa bila sababu ya msingi. Utakuta mmoja amenuna tu na asingependa kumuona mwenzie akimkaribia. Atapata furaha sana kama mwenzie hayupo lakini atachukia sana pale atakaporejea, akiulizwa kwa nini hana sababu zaidi ya kusema nimetokea kumchukia tu na hata natamani kutoka katika nyumba hii nikaishi mbali. Ndoa nyingi zimeingia katika migogoro mikubwa au kuvunjika kwa jinsi hii.
20. Kukosa usingizi. Tahadhari; ziko sababu nyingine za kibinadamu zinazoweza kusababisha hili ikiwemo magonjwa kama shinikizo la damu n.k, lakini pia huweza kusababishwa na msongo wa mawazo. Kama sababu hizi hazipo na mtu bado anakosa usingizi, hii itakuwa ni nguvu za giza kwa mtu husika.
21. Kuzuiwa wakati wa kuomba na kusoma neno la Mungu. Kila akijaribu kuomba au kusoma neno anakumbwa na uchovu au usingizi. Hii hufikia hatua hata mtu kuona giza pale anapoanza kusoma neno la Mungu. Anaweza hata asielewe anasoma nini kwa kuwa akili inakuwa imefungwa. Hata akiomba hasikii mguso wowote na anahisi hakuna muunganiko kati yake na mungu. Tahadhari isipochukuliwa athari zake uenea hadi kwenye ibada ya nyumbani ambapo watu karibia wote watasinzia kwenye ibada.
22. Kuona au kuota majitu ya kutisha au kupatwa na jinamizi. Mtu ataona majitu yasiyo ya kawaida ambayo yatamtisha binafsi hata kukosa amani kabisa. Wengine hupiga kelele kwa nguvu lakini watu wengine wakifika hawaoni chochote. Kwa wasiojua wanaweza kudhani kwamba anaanza kuchanganyikiwa.
23. Kusikia amebebeshwa vitu vizito mgongoni, kichwani au tumboni.
NAMNA WATU WANAVYOPATA NGUVU ZA GIZA
1. Ibada ya miungu. Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; name sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani. Hamwezi kushirikiana katika meza ya Bwana na meza ya mashetani 1Wakorintho 10:20-21. Ibada ya sanamu hufungulia milango mashetani kuingia kwako maana ni ibada yao. Baadhi ya ibada hizo ni kama za mazishi, tohara za kimila, harusi za kimila, utazamaji na usomaji wa vitu vinavyoendana na utukuzaji wa shetani n.k. ukifanya hivyo umejifungamanisha na miungu. Hivyo tahari ichukuliwe juu ya kila unachofanya, unachotazama, unachosikiliza na unachosoma; je vina mtukuza Mungu aliye hai au unafanya ibada ya mashetani bila kujua!! Nguvu za giza wakati mwingine huingizwa kwa kutamka maneno aidha kwa kusema, kusoma au kuimba. Ukitaka kuwa salama mkiri Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wako. Mwambie shetani mimi sasa ni wa Kristo, nimekukataa shetani na sihusiki na vitu vyako tena. Kumbuka waweza kuwa mshiriki wa kanisa na bado ukawa katika hali ya giza. Tamko rasmi linatakiwa la kumkataa shetani. Jifungie chumbani tamka kwa sauti wewe peke yako kwa ombio la dhati la kumkana shetani kwa maneno haya; “NIMEKUKATAA SHETANI NA SIHUSIKI NA VITU VYAKO TENA, MIMI SASA NI WA KRISTO”.
2. Kwa njia ya kimwili/matendo ya kimwili. Kama unatimiza tamaa za mwili unakaribisha nguvu za giza. Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambioa mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo, hawataurithi ufalme wa Mungu. Wagalatia 5:19-21
3. Kujiingiza katika dini na mafundisho ya uongo. Yule joka akatupwa, Yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye. Ufunuo 12:19. Baada ya kutupwa duniani, shetani alianza kuwadanganya wanadamu kwa kuwatoa katika kanuni takatifu za Mungu. Amechanganya kweli na uongo ili apate kujipatia wafuasi, kwa hila amejiingiza katika dini akijidai kulitaja jina la Yesu kana kwamba ni ibada ya Mungu huku kwa hakika wakimtukuza yeye. Maandiko ya Mungu yako bayana juu ya kanuni za Mungu wa kweli. Hivyo kama mtu ataamua kufuata dini za uongo matokeo yake ni kuukubali utawala wa shetani ndani yake. Hii humfanya aishi katika giza na kutegemea nguvu za giza pengine hata bila yeye mwenyewe kujua huku sala zake zikijibiwa na shetani.
4. Kutosamehe. Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji hata atakapoilipa deni ile yote. Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake. Mathayo 18:34-35. Kukiwa na ugumu wa mioyo kwa kushindwa kusamehe, mungu ataruhusu nguvu za giza zimwingie mtu kwa kuwa ataondoa ulinzi wake. Kanuni ya Mbinguni imesimama katika msamaha, lakini tabia ya shetani ni kisasi na uonevu. Hivyo kushindwa kusamehe ni kukubaliana na tabia ya shetani, hii ni sawa na kumkaribisha ndani kwako.
5. Kwa ruhusa ya Mungu. Basi, roho ya Bwana ilikuwa imemwacha Sauli, na roho mbaya kutoka kwa Bwana ikamsumbua. Nao watumishi wa Sauli wakamwambia, Angalia, sasa roho mbaya kutoka kwa Mungu inakusumbua. Basi bwana wetu na atuamuru sisi watumishi wake waliopo hapa mbele yako watafute mtu aliye stadi wa kupiga kinubi; basi itakuwa, roho ile mbaya kutoka kwa Mungu itakapokujilia, yeye atapiga kinubi kwa mkono wake, nawe utapona. 1Samweli 16:14-16. Neno lililo tumika katika mafungu haya roho mbaya kutoka kwa Bwana kwa kiebrania ilisomeka; roho chafu kwa idhini ya Bwana. Pale tunapozidi kuwa wakaidi Mungu huruhusu tupatwe na roho chafu kwa kuwa hatuko tayari kuisikia sauti yake. Waweza kujiuliza ni kwa nini alipigiwa kinubi? Je kinubi ni tiba ya roho wachafu? NDIYO; ukisoma kutayarisha njia sura 195 utakuta mjumbe wa Mungu akielezea juu ya matumizi ya muziki unaomtukuza Mungu; anasema … kuimba kama sehemu ya ibada ya dini ni sawasawa na ibada ya sala... Hivyo nyimbo zinazomtukuza Mungu zikiimbwa ni sawa na sala inayoweza kumfukuza shetani. Lakini endapo muziki utatumiwa vibaya huweza kumtukuza shetani hata kama kutatajwa jina la Yesu kila baada ya neno.
6. Kurushiwa mapepo. Kwa watu ambao hawajakubali sawasawa kafara ya Kristo na nguvu za Mungu juu yao hukosa ulinzi wa Mungu; hivyo huwa rahisi kutupiwa mapepo na mawakala wa shetani waliotapakaa duniani kote.
7. Kurushiwa au kutumia vitu vyenye asili ya shetani. Mavazi, vipodozi na vito vimekuwa ni chanzo kikubwa cha watu kupata nguvu za giza. Yeye mwenyewe, shetani na mawakala wake wamekuwa wabunifu wa mitindo mbali mbali ya uvaaji ambavyo ndani yake mna mapepo yanayowaingia watu na kukaa kwao. Wakati mwingine vitu hivi watu hupewa na waganga kwa imani za kishirikina, ikiwemo irizi, tunguri n.k. hivi vyote humtukuza shetani kwa kuwa ndiyo dini yake; yeye akiwa mkuu wake.
SABABU ZA PEPO KUMTOKA MTU NA KURUDI TENA
1. Kutochukua hatua ya toba ya dhati kutoka moyoni.
2. Kuendelea kutenda dhambi/kutoacha dhambi. Zingatia si kila aliyerudiwa na mapepo ana dhambi! Lakini ni jambo la msingi sana kuacha dhambi ili roho wa Bwana atawale ndani yako kweli kweli, isipokuwa hivi utamruhusu shetani na nguvu zake kutawala ndani yako na kukufanya kuwa himaya yao.
3. Mwendelezo wa kuwa na vitu, mikataba au maagano na ulimwengu wa giza. Kama mtu atakuwa ameshindwa kuvunja mikataba na shetani au kuacha vitu vya nguvu za giza bila shaka hata kama ataombewa nguvu za giza zitamrudia tena maana bado zina nafasi ndani yake.
4. Kutoamini, uoga, mashaka na hofu. Tembea kwa imani huku ukiamini utendaji wa Mungu na Roho wake aliye ndani yako. Ondoa hisia za kushindwa, hata kama utasikia kitu fulani kikiwa hakiko katika hali yake ya kawaida mwilini mwako, wewe sisitiza ushindi katika damu ya Yesu. Kumbuka lolote utakalolitamka kwa imani kwa mapenzi ya Mungu itakuwa hivyo. Kuwa na mashaka juu ya utendaji wa Mungu aliye mkuu kuliko vyote ni kupungukiwa na imani juu yake. Hii hufanya mtu husika kukaribisha nguvu za giza kwa maneno yake ya kukata tama juu ya miujiza ya Mungu aliye chanzo cha vyote. WEWE TAYARI NI MSHINDI KWA NINI UOGOPE!!
5. Kuendeleza imani juu ya wale waliotamkwa na mapepo kwamba ndio wanaomshambulia! Ni kosa kubwa sana kuwa na chuki juu ya mtu, kwa kuwa huwezi kuwa na hakika kama anachokisema shetani ni ukweli. Hata kama ni kweli unapaswa kumsamehe na kumuombea ili nguvu za giza zimtoke akate shauri na kuokolewa. Zingatia kuwa wachawi wanaweza kutenda wao wenyewe au kuvaa sura ya mtu mwingie asiyehusika ili kukuchonganisha naye halafu yeye akaendelea kutojulikana, lakini pia mizimu nayo huvaa sura za watu, hivyo mapepo yanaweza kumtamka mtu asiyehusika kwa kuwa sura yake ndiyo inayoonekana kwa kutumiwa na nguvu za giza kama chambo tu. Kama mtu ataendelea kujenga chuki na fitina, hakika nguvu za giza zitamrudia.
NAMNA YA KUMSAIDIA MTU ALIYEINGIWA NA NGUVU ZA GIZA
1. Mjenge katika kuwa mtu wa maombi yeye binafsi, aweze kupambana katika jina la Yesu bila kutegemea msaada pekee kutoka kwa wana maombi au mtu mwingine. Mjenge katika misingi ya yeye mwenyewe kujenga daraja lisilokatika kati yake na Mungu Mkuu. Hii itamuongezea imanai kwa uzoefu huu atakuwa ameshinda nay eye kuwa mtu wa kushauri na kusaidia katika kuwaombea wengine.
2. Mjenge katika misingi ya kusoma neno la Mungu mara kwa mara na kujifunza tabia ya Mungu kwa bidii. Maneno ya Mungu aliye hai yanapotamkwa ndani ya mtu mara kwa mara shetani hukimbia asikaribie tena, maana hii ndiyo silaha kubwa ya kumshinda. Kwa kusoma neno la Mungu mtu hupata fursa ya kuongea nay eye mwenyezi moja kwa moja. Neno litamburudisha na kumfariji na kujisikia amani na mshindi wakati wote.
3. Ulaji, unywaji, uvaaji, usomaji, usikilizaji na utazamaji wake uwe katika mwelekeo wa kumtukuza Mungu. Msaidie aepuke kutazama, kusikiliza au kusoma mambo yanayomtukuza shetani; ikiwemo tamthilia, magazeti na vitabu vya ajabu ajabu n.k. msaidie pia katika kubadilisha mtindo wa kula, kunywa na kuvaa. Mungu wetu ameweka utaratibu mzuri wa kufanya yote kwa utukufu wake. Mshauri aepukane na vipodozi vya ajabu, mavazi yasiyositiri mwili hasa kwa wanawake. Kumbuka muhasisi na mbunifu mkuu wa mambo hayo ni Ibilisi.
4. Mjenge katika imani kwa Mungu akiondoa hofu na mashaka juu ya utendaji wa Mungu. Mjenge katika kukiri ushindi kila wakati; asiwe mtu wa kutilia mashaka alichotendewa na Mungu. Shetani ujaribu kuwatia watu hofu ili awaondolee amani na imani yao kwa Mungu. Shetani kwa hakika hufurahi sana anaposikia watu wakijadili namna ya anavyo fanya kazi kwa kufanikiwa. Endapo utalalamika kila wakati na kusahau nguvu za Mungu zilizo ndani yako na kushindwa kumtukuza Mungu na kumkemea shetani, utampa mwovu mwanya wa kukushambulia kwa udhaifu huo. Waweza kusema “NAMSHUKURU MUNGU MKUU KWA MAANA KILA WAKATI SHETANI ANASHINDWA”.
5. Msaidie aepuke vyanzo vinavyoleta nguvu za giza; mfano ushirikina, ramli, mavazi, vipodozi n.k. shetani upendelea kuona watu wakijihusisha katika hivi vitu maana vinamtukuza.
6. Msaidie ajiepushe na mafundisho na dini za uongo. Maana huko pia shetani hujitukuza na kuwaingia watu wakidhani wamepata Roho wa Mungu na kumbe wamepagawa na nguvu za giza wakipiga makelele na kuzungumza maneno yasiyoeleweka. Kuendelea kuwepo huko ni kuendelea kumkaribisha shetani.
7. Msaidie ajiepushe na imani juu ya wale wanaomshambulia ikiwa imetokea kwa bahati mbaya akaelewa. Kama hakusikia mapepo yakiongea basi wale wanaomuombea hawapaswi kabisa kumwambia, maana kwa walio wengi watajenga chuki na fitina itakayofanya shetani aendelee kukaa ndani yao.
8. Mjenge katika kuimba nyimbo zinazomtukuza Mungu na kuacha kabisa zile zinazomtukuza ibilisi. Kumbuka nyimbo pia ni ibada sawa na ibada ya sala. Kumbe kuimba kutamfanya awe anawasiliana na Mungu wakati wote na kumfukuza yule adui
9. Msaidie atambue nguvu ya damu ya Yesu katika kuokoa, kusafisha na kumshinda mwovu. Mada hii inajadiliwa kwa kina katika vipengele vinavyofuata.
NGUVU KATIKA DAMU
1. Waebrania 12:24 na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili. Damu ya Habili ilipomwagika na kulia juu ya ardhi, matokeo yake ilikuwa ni nguvu iliyosababisha ardhi kulaaniwa! Lakini damu ya Yesu Kristo yenyewe ilipomwagika, nguvu yake ilimfunika mwanadamu kutoka katika mauti na kuwa na tumaini la uzima wa milele. Ilimpa mwanadamu asiyesitahili nafasi nyingine ya kumuona muumba wake, ilimpa mwanadamu mnyonge na mdhaifu nguvu za kukanyaga nge na nyoka bila madhara na kumshinda yule mwovu kwa mamlaka ya damu ya Kristo. HAKIKA DAMU YA YESU YATOSHA.
2. Mwanzo 2:7 BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai. Kumbe uhai wa mtu ulitokana na kupuliziwa pumzi ya uhai ndani yake. Jambo la msingi ili mwanadamu awe hai ni kuwa na kitu kinacholeta uhai ndani yake. Je uhai wa mwanadamu uko wapi? Mambo ya Walawi 17:10-11 kisha mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli, au miongoni mwa hao wageni wakaao kati yao, atakaye kula damu ya aina yoyote, nitakunja uso wangu juu ya mtu huyo alaye damu, nami nitamkatilia mbali na watu wake. Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho juu kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi. Ooh kumbe uhai wa mwanadamu uko katika damu ambayo pia hufanya upatanisho kati ya Mungu na wanadamu waliotenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu. Ikiwa damu ya mnyama yaweza kuwa na nguvu kiasi hiki katika upatanisho; je si zaidi kwa damu ya Yesu? Ndiyo maana leo tunayo mamlaka ya kumshinda mwovu kwa sababu ya nguvu ya damu ya Yesu Kristo iliyomwagika kwa ajili yetu. HAKIKA WEWE NI MSHINDI KATIKA DAMU YA KRISTO.
3. Vielelezo halisi vya maagano, upatanisho na kufunikwa na nguvu ya damu. Mwanzo 3:7 wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mti, wakajifanyia nguo. Baada ya anguko mwanadamu alitafuta namna ya kujifunika kwani tayari ilishapungukiwa na utukufu wa Mungu. Jitihada zao hazikuweza kuleta ufunikwaji halisi kwa kuwa walitumia miti ambayo ndani yake hapakuwa na nguvu yoyote. BWANA Mungu akafanya mpango wa kuwafunika; Mwanzo 3:21 BWANA Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika. Kwa mara ya kwanza katika historia ya dunia, damu ilimwagika kwa ajili ya kumfunika mwanadamu aliyepungukiwa na utukufu wa Mungu. BWANA mwenyewe alihusika katika matumizi ya damu kwa ajili ya watu wake. Mwanzo 8:20 Nuhu akamjengea BWANA madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliyesafi na katika kila ndege aliyesafi,akavitoa sadaka ya kuteketezwa juu ya madhabahu. Mwanzo 17:10 hili ndilo agano langu utakalolishika, kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, kila mwanamume wa kwenu atatahiriwa. Hili lilikuwa agano kati ya Mungu na Ibrahimu na uzao wake wote. Ni agano linalohusika na umwagikaji wa damu katika huduma ya tohara. Mwanzo 31:54 Yakobo akachinja sadaka katika mlima, akawaita ndugu zake waje wale chakula, nao wakala chakula, wakakaa usiku kucha mlimani. Kutoka 24:5-8 akapeleka vijana wa wana wa Israeli, waliotoa sadaka za kuteketezwa, wakamchinjia BWANA sadaka za amani za ng’ombe. Musa akatwaa nusu ya ile damu, akaitia katika mabakuli; na nusu ya ile damu akainyunyiza juu ya madhabahu. Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa wtu; wakasema, hayo yote aliyoyanena BWANA tutayatenda, nasi tutatii. Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, hii ndiyo damu ya agano alilolifanya BWANA pamoja nanyi katika maneno haya yote. Kwa damu Mungu aliye mkuu anafanya mapatano yenye ahadi na wanadamu!
Waebrania 11:4 kwa imani Habili alimtolea Mungu dhabihu iliyo bora kuliko Kaini; kwa hiyo alishuhudiwa kuwa ana haki; Mungu akazishuhudia sadaka zake, na kwa hiyo ijapokuwa amekufa angali akinena. BWANA aliikubali sadaka ya Habili kwa kuwa alitoa kwa mpango wa Mungu yaani mnyama. Damu ilitakiwa kufanya upatanisho kati ya Mungu na Habili. Kaini alikataliwa kwa sababu alitoa kinyume na mpango wa Mungu. Alitoa mazao yasiyokuwa na damu, hivyo hakupata utakaso. Vielelezo hivi vyote vinatuonyesha nguvu ya damu katika kufanya maagano na kutakaswa na Mungu aliye mkuu. Sasa tuone nguvu katika damu ya Yesu.
ULINZI KUPITIA DAMU YA YESU
1. Kutoka 11:4-5 Musa akasema, Bwana asema hivi, Kama usiku wa manane mimi nitatoka nipite kati ya Misri; na wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri watakufa, tangu yule mzaliwa wa kwanza wa Farao aketiye katika kiti chake cha enzi, hata mzaliwa wa kwanza wa huyo kijakazi aliye pale nyuma ya jiwe la kusagia; na wazaliwa wa kwanza wote wa wanyama. Kutoka 12:12-13 Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi Bwana.
Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri. Kama ilivyotumika kuwafunika wana wa Israeli wasipatwe na mabaya ndivyo damu ya Kristo inavyotufunika sisi na kutupatia ulinzi imara pale tunapokiri na kukubali kwa dhati kuwa inayo nguvu ya kutulinda.
2. Ufunuo 12:10-1110 Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku. Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa. Walioshinda na watakaoshinda katika ulimwengu wa leo ni wale tu watakaokuwa chini ya damu iokoayo ya Yesu Kristo. Huna sababu ya kuwa na hofu wala shaka ndani yako maana tayari damu ya Mwana-Kondoo wa Mungu ipo kwa ajili yako; hakuna litakalokushinda katika ulimwengu huu.
3. Ayubu 1:5,10 Basi ilikuwa, hapo hizo siku za karamu zao zilipokuwa zimetimia, Ayubu hutuma kwao akawatakasa, kisha akaamka asubuhi na mapema, na kusongeza sadaka za kuteketezwa kama hesabu yao wote ilivyokuwa; kwani Ayubu alisema, Yumkini kwamba hawa wanangu wamefanya dhambi, na kumkufuru Mungu mioyoni mwao. Ndivyo alivyofanya Ayubu sikuzote. Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi. Pamoja na kutakasa, damu ya yesu pia uweka wigo/ulinzi usiotikisika wala kuteteleka kwa watu wake.
4. 1Yohana 4:4 Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia. Kwa kuwa tulipuliziwa pumzi ya uhai ambayo iko ndani yetu, ambapo uhai hutokana na damu ambayo tayari ilishamwagika kwa ajili yetu yaani Yesu Kristo; twaweza kusema kuwa Kristo anaishi ndani yetu kupitia damu yake. Kwa kuwa yeye anazo nguvu kuliko mwovu nasi tumemshinda yule adui katika Krito maana Kristo anakaa ndani yetu.
MAKOSA YA WAOMBAJI WENGI KATIKA MATUMIZI YA DAMU YA YESU
Ni kosa kusema pepo kunywa damu ya Yesu. Shetani hawezi kuokoka tena hivyo hawezi kunywa damu ya Yesu inayookoa. Hii sentensi imekuwa ikitumika kimakosa pengine kwa kutokujua matumizi ya damu ya Yesu! Kristo alimwaga damu yake kwa ajili ya watu wote hasa wale watakaokuwa tayari kuupokea wokovu wake. Mathayo 26:26-28 Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu. Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. Kwa mafungu haya utagundua kuwa damu ya Yesu ni kwa ajili ya washindi na watakatifu si ya kunywa mapepo yasiyokuwa na tumaini la wokovu.
USHAURI
Jitahidi kusoma neno la Mungu mara kwa mara na kuomba maana hii ni njia mojawapo ya kuongea na Mungu. Miongoni mwa sura utakazosoma waweza pia kusoma Zaburi 35 kwa ajili ya faraja na ushindi. Hebu tazama sura hii inavyokufaa:
Ee Bwana, utete nao wanaoteta nami, Upigane nao wanaopigana nami. Uishike ngao na kigao, Usimame unisaidie. Uutoe na mkuki uwapinge wanaonifuatia, Uiambie nafsi yangu, Mimi ni wokovu wako. Waaibishwe, wafedheheshwe, Wanaoitafuta nafsi yangu. Warudishwe nyuma, wafadhaishwe, Wanaonizulia mabaya. Wawe kama makapi mbele ya upepo, Malaika wa Bwana akiwaangusha chini. Njia yao na iwe giza na utelezi, Malaika wa Bwana akiwafuatia. Maana bila sababu wamenifichia wavu, Bila sababu wameichimbia shimo nafsi yangu. Uharibifu na umpate kwa ghafula, Na wavu aliouficha umnase yeye mwenyewe; Kwa uharibifu aanguke ndani yake. Na nafsi yangu itamfurahia Bwana, Na kuushangilia wokovu wake. Mifupa yangu yote itasema, Bwana, ni nani aliye kama Wewe? Umponyaye maskini na mtu aliye hodari kumshinda yeye, Naam, maskini na mhitaji na mtu amtekaye. Mashahidi wa udhalimu wanasimama, Wananiuliza mambo nisiyoyajua. Wananilipa mabaya badala ya mema, Hata nafsi yangu ikaingia ukiwa. Bali mimi, walipougua wao, Nguo yangu ilikuwa gunia. Nalijitesa nafsi yangu kwa kufunga; Maombi yangu yakarejea kifuani mwangu. Nalijifanya kama kwamba ni rafiki au ndugu yangu, Naliinama nikilia kama aliyefiwa na mamaye. Lakini nikijikwaa hufurahi na kukusanyana, Walinikusanyikia watu ovyo nisiowajua, Wananipapura wala hawakomi. Kama wenye mzaha wakikufuru karamuni Wananisagia meno. Bwana, hata lini utatazama? Uiokoe nafsi yangu na maharabu yao, Na mpenzi wangu na wana-simba. Nitakushukuru katika kusanyiko kubwa; Nitakusifu kati ya watu wengi. Walio adui zangu bure wasinisimange, Wanaonichukia bila sababu asining'ong'e.
Maana hawasemi maneno ya amani, Na juu ya watulivu wa nchi huwaza hila. Nao wananifumbulia vinywa vyao, Husema, Ewe! Ewe! Jicho letu limeona. Wewe, Bwana, umeona, usinyamaze; Ee Bwana, usiwe mbali nami. Uamke, uwe macho ili kunipatia hukumu Kwa ajili ya madai yangu, Mungu wangu na Bwana wangu. Unihukumu kwa haki yako, Ee Bwana, Mungu wangu, Wala wasinisimangize. Wasiseme moyoni, Haya! Ndivyo tutakavyo; Wasiseme, Tumemmeza. Waaibishwe, wafedheheshwe pamoja, Wanaoifurahia hali yangu mbaya. Wavikwe aibu na fedheha, Wanaojikuza juu yangu.
Washangilie na kufurahi, Wapendezwao na haki yangu. Naam, waseme daima, Atukuzwe Bwana, Apendezwaye na amani ya mtumishi wake. Na ulimi wangu utanena haki yako, Na sifa zako mchana kutwa.

Share:

Popular Posts

Total Pageviews

Search This Blog

Powered by Blogger.

Search This Blog

AUDIO

About Me

My photo
Nyamagana City, Mwanza, Tanzania

Labels

Recent Posts